Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Oktoba, 2021 amezindua Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu (The Tanzania Gender Bench Book on Women’s Rights) nchini Tanzania kuhusu haki za wanawake, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Samia amesema Kitabu hicho ambacho kimeandaliwa na wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) kwa hisani ya UN Women na Ubalozi wa Sweden, kitakuwa msaada mkubwa sio tu kwa wanawake na watoto bali kwa jamii nzima hususan katika masuala ya haki.
Mhe. Rais Samia amewapongeza TAWJA kwa kuandaa kitabu hicho kinachotoa muongozo wa namna ya kulinda haki za wanawake na watoto pamoja na kukuza utawala wa sheria hapa nchini.
Mhe. Rais Samia amesema Kitabu hicho pamoja na mambo mengine, kitatoa rejea rafiki na ya haraka kwa lengo la kuwarahisishia watoa maamuzi kulinda haki za wanawake na watoto.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema mwongozo huu utasaidia kuongeza dhamira na nia ya dhati ya kuimarisha muitikio chanya wa masuala ya kijinsia katika maamuzi ya Mahakama na vyombo vingine vinavyoshughulika na utoaji haki.
Mhe. Rais Samia amesema Kitabu hiki kimekuja wakati muafaka ambapo Mahakama imeshakamilisha ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kwa maswala ya familia.
Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu wote wanaoshughulikia mashauri ya kutelekeza, mirathi, dhuluma, udhalilishwaji na unyanyaswaji kutumia kitabu hicho kama miongoni mwa miongozo itakayotumiwa na Mahakama ya masuala ya familia.
Mhe. Rais Samia amesema ana imani kuwa kitabu hicho kitasaidia kuibua haki nyingi za wanawake na watoto zinazojulikana kwa watu wengi na zile ambazo hazijulikani na walio wengi. Pia kitasaidia kuwapa watoa haki ujasiri wa kutoa maamuzi yatakayopelekea kuzika baadhi ya mila, desturi na imani potofu zinazokandamiza na kupora haki za makundi muhimu katika jamii.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha anajenga nchi inayoheshimu na kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora kwa maendeleo ya wote kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Mhe. Rais Samia amewaomba TAWJA na wadau wote walioshiriki katika uandaaji wa Kitabu hiki kuhakikisha kuwa kitabu hicho kinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo inaeleweka kwa wengi hususan kwenye mifumo ya utoaji haki.
Pia Mhe. Rais Samia amesisitiza kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika mienendo ya mashauri na hukumu kwasababu tayari Bunge lilishafanya marekebisho ya Sheria kuruhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sheria hapa nchini.