Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 13 Novemba, 2021 amepokea kifimbo cha Malkia wa II wa Uingereza kutoka kwa Mratibu wa Kifimbo hicho hapa nchini Bw. Henry Tandau, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kifimbo hicho kinapita nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola kuashiria uzinduzi wa michezo ya Jumuiya hiyo itakayofanyika Birmingham nchini Uingereza mwaka 2022.
Mhe. Rais Samia ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Kamati ya Olimpiki Tanzania kwa kumpa heshima ya kupokea kifimbo hicho.
Aidha, amesema kuwa anatambua Tanzania imekuwa mwanachama na mshiriki mzuri wa michezo ya Jumuiya ya Madola bila kukosa tangu mwaka 1962 ambapo imefanikiwa kushinda jumla ya medali za dhahabu 6, fedha 6 na shaba 9.
Mhe. Rais Samia amewataka wanamichezo wote watakaopata nafasi kutoka Tanzania kuhakikisha wanarudi na medali kwa sababu tangu tulipoanza kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola hatujawahi kurudi bila kupata medali isipokuwa katika michezo mitatu ya mwisho ya mwaka 2010, 2014 na 2018.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amesisitiza kuwa michezo ya Jumuiya ya Madola ina ushindani mkubwa hivyo huhitaji wanamichezo mahiri na waliojiandaa na kuandaliwa ipasavyo.
Mhe. Rais Samia ameagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kusimamia kikamilifu maandalizi ya michezo hiyo ili nchi iweze kurejesha medali zilizopoteza kwa muda mrefu.
Pia, Mhe. Rais Samia amewataka wachezaji na walimu wa timu zitakazokwenda kushiriki katika michezo hiyo kuhakikisha kuwa wanajituma na kuonesha weledi mkubwa ili waweze kupambania taifa kushinda medali.
Ameitaka Kamati ya Olimpiki Tanzania iwasilishe mapema mpango wake Wizarani ili ijadiliwe na kuangalia uwezekano wa kuingizwa kwenye mipango ya bajeti ijayo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kuwa ujio wa Kifimbo cha Malkia ni fursa kubwa kwa nchi yetu kujitangaza na kujitambulisha duniani kwasababu kina kamera inayowezesha maeneo kinapopita kuonekana duniani kote na hivyo kutupatia fursa ya kuvutia watalii na wawekezaji mbalimbali.
Mhe. Rais Samia amewakumbusha vyama vya michezo kuwa wabunifu na kuwaandaa wachezaji wao ipasavyo ili yasijirudie yaliyotokea katika Olimpiki nchini Japan ambapo walipelekwa wachezaji wa mbio ndefu pekee.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amesema licha ya timu ya Taifa Stars kupoteza matumaini ya kwenda kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar, hawapaswi kukata tamaa kwa kuwa bado kuna nafasi ya kushinda mechi ijayo na kuipa heshima Tanzania kufikia hatua ya kumaliza nafasi ya pili ya kundi letu.