TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 14 Novemba, 2021 amezindua jengo jipya la Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es Salaam, lililojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa China kwa gharama ya shilingi bilioni 57.

Mhe. Rais Samia amesema China na Tanzania zina historia ya muda mrefu na ni marafiki muhimu katika nyanja mbalimbali za maendeleo pamoja na shughuli za kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata kijeshi.

Mhe. Rais Samia amesema mbali na ushirikiano uliopo katika nyanja mbalimbali, Serikali ya Watu wa China imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kutupatia misaada ambayo inalijengea Jeshi letu uwezo wa mafunzo kwa vitendo katika nyanja za kimedani, kutupatia vifaa, fedha pamoja na miradi mingine.

Pia, Mhe. Rais Samia amesema Ujenzi wa Chuo hicho umelisaidia Jeshi na Taifa kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kusomesha wanafunzi nje ya nchi badala yake hivi sasa Serikali itaelekeza fedha hizo kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

Mhe. Rais amesema kupata majengo ni hatua moja katika kuboresha elimu katika sekta ya Ulinzi na Usalama nchini, hivyo mitaala itakayofundishwa na mbinu za utoaji mafunzo ni lazima ziendane na wakati na zikidhi mahitaji ya fani husika.

Vilevile, amesema kupitia Chuo hicho Serikali imeweza kupata watendaji wazuri wenye weledi na uthubutu wa kufanya maamuzi yenye kuzingatia maslahi ya taifa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama na hatimaye kupiga hatua kubwa katika kujiletea maendeleo.

Mhe. Rais Samia ameishukuru Serikali ya Watu wa China kwa msaada wa majengo hayo ambayo amesema yatasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa pia kutoa fursa kwa Chuo hicho kutoa mafunzo mengi zaidi.

Aidha, Mhe. Rais Samia amezipongeza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana vizuri kuwezesha kukamilika kwa majengo hayo na kutoa wito kwao kuendelea kuimarisha urafiki na uhusiano kati ya China na Tanzania kwa manufaa endelevu kwa taifa.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi, Mhe. Rais Samia pia ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makabidhiano ya jengo hilo kati ya Serikali ya Tanzania na China.

 Hafla ya uzinduzi wa Jengo la chuo cha NDC imehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Majeshi Wastaafu, Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa Meja Jenerali Ibrahimu Mhona na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania na China.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *