TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi nchini kubadilika na kuzingatia taratibu na maadili ya Jeshi hilo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Mhe. Rais Samia ametoa maagizo hayo tarehe 12 Desemba, 2021 wakati akifunga Mafunzo ya Uofisa Kozi Na. 01/2020/2021 (Warakibu Wasaidizi wa Polisi – ASP) katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amesema vitendo vya rushwa na askari kujiona kuwa na nguvu isiyohojiwa kwa wananchi huliondolea Jeshi hilo uaminifu kwa wananchi wanyonge.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametolea mfano wa matukio kadhaa aliyokumbana nayo kipindi cha nyuma wakati akiwa Kiongozi  Serikalini na kuhoji namna hali ilivyo kwa wananchi wa kawaida ikiwa yeye kiongozi alikutana na vitendo hivyo vya rushwa. Amesema vitendo hivyo vinashusha imani kwa wananchi, hivyo Jeshi la Polisi wanatakiwa kurekebisha hali hiyo ili kurudisha imani kwa wananchi.

Kuhusu kuwapandisha vyeo askari wa Jeshi hilo, amesema Serikali imepandisha vyeo maafisa, wakaguzi na askari polisi, kuajiri askari mbadala na askari wapya wapatao 4103, kuipandisha hadhi Hospitali ya Polisi iliyopo barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Mhe. Rais Samia amesema ni matumaini yake kuwa maboresho hayo yataleta matokeo chanya katika utendaji kazi wa Jeshi la Polisi na kutoa huduma zenye ubora na weledi kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema amefurahishwa na ongezeko la idadi ya wahitimu ambao wamefikia 749 ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 370 mwaka 2009.  

Mhe. Rais Samia ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha doria kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi ili kuhakikisha vitendo vya kihalifu kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka vinadhibitiwa.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya uhalifu ili wananchi wachukie vitendo vya uhalifu na wahalifu.

Mhe. Rais Samia amesema amani na usalama ndio misingi ya maendeleo katika nchi, hivyo amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha shughuli zote za maendeleo, kiuchumi, kisiasa, kijamii na uzalishaji zinafanyika bila hofu wala bughudha.

Kuhusu suala la silaha, Mhe. Rais Samia amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kulipa kipaumbele kwa kuwataka wananchi kurudisha silaha wanazomiliki kinyume na sheria.

Mhe. Rais Samia amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza uhalifu mitaani na kuitaka polisi kuendelea kuwachukulia hatua wananchi wachache ambao hawataki kubadilika.

Amewataka wahitimu wote kutambua kuwa kazi kubwa mbele yao ni utendaji kazi wenye matokeo chanya kwao, Serikali na jamii kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *