Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka Wizara zilizogawanywa zianze kujipanga kimuundo na kuanza utekelezaji wa majukumu yake mara moja.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 10 Januari, 2022 mara baada ya kuwaapisha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro katika hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema tarehe 13 Januari, 2022 anatarajia kuzungumza na Mawaziri na Naibu Mawaziri walioapishwa Mkoani Dodoma.
Mhe. Rais Samia amesema licha ya kuwaacha katika uteuzi Mawaziri wawili Mhe. Palamagamba Kabudi aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mhe. William Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ataendelea kuwatumia ili waweze kumsaidia kusimamia viongozi aliowateua kutekeleza majukumu yao.
Hafla hiyo ya Uapisho imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania Mhe.Tulia Ackson, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma pamoja na viongozi wengine wa Chama na Serikali.