TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu amesema Tanzania inaendelea kufurahia amani na utulivu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Mhe. Rais amesema hayo tarehe 24 Januari, 2022 wakati akizungumza na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika sherehe za mwaka mpya 2022 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) zilizofanyika katika Ukumbi wa Kikwete Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema hali ya amani nchini inatoa fursa kwa Serikali kuelekeza nguvu zake katika kuimarisha uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema katika kuimarisha demokrasia nchini, Serikali imeendelea kuruhusu uhuru wa kujieleza kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kurekebisha Sera ya Mambo ya Nje ili kuakisi mabadiliko na maendeleo mapya duniani.

Pia, Mhe. Rais Samia amesema Sera mpya ya mambo ya nje itaendelea kuzingatia diplomasia ya uchumi na kuakisi maendeleo mapya kama vile uchumi wa buluu, mabadiliko ya tabianchi, uchumi wa kidijitali pamoja na kukuza lugha ya Kiswahili kama lugha ya kidiplomasia na kibiashara.

Mhe. Rais Samia ameshukuru wale wote waliopitisha maazimio ya kuifanya tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa siku ya lugha ya Kiswahili duniani.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema, anaridhishwa na maendeleo yanayofanywa na Tanzania katika kukuza ushirikiano na nchi zilizo na wawakilishi wake hapa nchini, hivyo kama taifa linatoa kipaumbele kwa uhusiano uliopo kwa sababu nchi hizo zinaiwezesha Tanzania kutekeleza ajenda za maendeleo.

Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania ina imani na mahusiano ya Jumuiya za Kikanda katika kutatua changamoto za kikanda na kufikia matarajio ya pamoja katika maeneo ya amani na usalama, demokrasia, biashara na uwekezaji, miundombinu pamoja na sekta za kijamii.

Mhe. Rais Samia amesema biashara ni muhimu katika ushirikiano wa kikanda hivyo Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa washirika wa biashara wa kikanda.

Kuhusu janga la UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amesema bado Tanzania inaendelea kufuata miongozi na itifaki ya Shirika la Afya Dunia (WHO) katika kukabiliana na maambukizi ya wimbi jipya la virusi vya UVIKO na inaendelea na kampeni ya kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19.

Pia, Mhe. Rais Samia ameziomba nchi ambazo Mabalozi wake wamehudhuria sherehe hiyo, kuhakikisha kunakuwa na usawa wa chanjo na kuondolewa kwa hati miliki ili kumudu kuzalisha chanjo zetu  wenyewe.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amesema licha ya kushuka kwa uchumi kutoka 7% mwaka 219 hadi 4.8% mwaka 2020 kutokana na janga la UVIKO 19, uchumi wa Tanzania uliongezeka na kufikia 4.9% mwaka 2021 na vipo viashiria kwamba uchumi unaendelea kuimarika.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema mfumuko wa bei nchini Tanzania ni asilimia 3-5 kwa mwaka 2021/2022 ambayo inawiana na vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari na serikali imeshajenga jumla ya vyumba 15,000 vya madarasa ambapo vyumba 3000 ni kwa ajili ya shule za msingi na 12,000 kwa ajili ya shule za sekondari.

Mhe. Rais Samia amesema katika kutekeleza ajenda ya maendeleo shirikishi, Serikali imewarejesha shuleni wanafunzi wakike waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito ili kufikia lengo namba 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kuhusu ujenzi wa miradi mikuu ya miundombinu, Mhe. Rais Samia amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara, reli, usafiri wa anga na majini, na miradi mikubwa ya nishati ambayo inaungwa mkono na baadhi ya nchi zenye balozi zake hapa nchini.

Mhe. Rais Samia amewatakia Heri ya Mwaka Mpya 2022 Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Viongozi Wakuu wa Nchi hizo katika Sherehe za Mwaka Mpya 2022 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *