Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Sekta ya Sheria na Utoaji wa Haki nchini kuangalia namna bora ya kutayarisha wahitimu na kuongeza maarifa kwa wanasheria walio kazini yaendane na wimbi la ukuaji wa teknolojia ya TEHAMA, ili nchi iweze kunufaika na matumizi ya teknolojia hiyo.
Mhe. Rais Samia ametoa wito huo leo tarehe 02 Februari, 2022 wakati akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini, Dodoma.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kuwa dunia ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambayo yanaongozwa na sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hivyo uchumi wa dunia pamoja na shughuli mbalimbali zinaendeshwa kwa kutumia TEHAMA.
Mhe. Rais Samia amezitaka Wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Vyuo Vikuu vyote kuhakikisha kuwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu wanapatiwa ujuzi utakaowaandaa kufanya kazi zinazohitaji ujuzi unaolingana na matakwa ya mabadiliko ya teknolojia.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema wakati tulionao unahitaji mabadiliko makubwa ya kifikra na kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi linganifu na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Mhe. Rais Samia amewapongeza viongozi wa sekta ya Sheria kwa hatua zinazochukuliwa ikiwemo kutafuta teknolojia yenye programu za kisasa ambazo zitaimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kutoa huduma za kimahakama na kutoa nafasi kwa lugha ya Kiswahili kupata tafsiri na unukuzi (transcription) kwa lugha ya Kiingereza na lugha zingine za kigeni.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema Serikali ipo tayari kutumia njia za kisasa katika kujenga uwezo na uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani katika masoko ndani ya Kanda zetu za Afrika na Duniani kwa ujumla.
Amesema, Tanzania haiwezi kubaki nje ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambayo yanaendelea kubadilisha mizani ya ushindani katika shughuli zote za kibinadamu, zikiwemo za uwekezaji na mazingira ya biashara.
Mhe. Rais Samia amesema ili kufanikisha lengo hilo ni lazima kuiboresha sekta ya Sheria na Utoaji wa Haki nchini, ili iweze kukabiliana na migogoro na mashauri ya kibiashara, na kutoa ufafanuzi wa kisheria katika masuala ya uwekezaji na biashara wakati wowote.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Mahakama kuzingatia Sheria na Katiba ya nchi na kutenda haki kwa watu wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi bila kucheleweshewa au kunyimwa haki wananchi kwa kufungwa na masharti ya kiufundi.