TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi ili kurahisisha utambuzi wa wakazi na makazi katika kuleta maendeleo endelevu nchini.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 08 Februari, 2022 katika Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Mhe. Rais Samia amesema lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na Anwani ya Makazi katika eneo lake analoishi, kaya, ofisi ama eneo la biashara ili kuweza kuhudumiwa kwa ufanisi.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema mfumo huo wa utambuzi ni bora na unaendana na mabadiliko ya uchumi wa kidijitali duniani hivyo ni muhimu katika zama hizi ambazo watu wanatumia TEHAMA katika shughuli mbalimbali za mawasiliano kijamii na kibiashara.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa kukosekana kwa mfumo wa uhakika wa utambuzi wa wakazi na makazi, kumekuwa na athari nyingi za kiuchumi, kiusalama na kijamii.  

Pia, Mhe. Rais Samia amesema Mfumo wa Anwani za Makazi una tija kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kuwezesha kufanyika kwa biashara mtandao, kuimarisha ulinzi na usalama, kuongeza mapato na kuongeza ajira.

Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeshaandaa Postikodi (anwani za kijiografia) na zimegawiwa kwa Kata zote nchini kwa ajili ya kutambua makazi na hivi sasa wanakusanya taarifa za wakazi na kuweka miundombinu ya majina ya mitaa na namba za nyumba.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Sekta zote nchini kuibua, kuwajengea uwezo na kuwatumia wataalamu watanzania katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohitaji taaluma walizonazo kama ilivyofanyika katika Programu Tumizi (Mobile App) ya anwani za makazi.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameelekeza Wakuu wa Mikoa kukamilisha zoezi la Anwani za Makazi kufikia mwezi Mei, 2022 na zoezi hilo lifanyike kama operesheni maalum katika muda uliopangwa ikijulikana kama Operesheni Anwani za Makazi.

Mhe. Rais Samia amewatahadharisha Wakuu wa Mikoa kuwa fedha za mradi huo sio za matumizi ya Ofisi (OC) bali ni kwa ajili ya mradi huo na kuzitaka Halmashauri nchini kuchangia fedha kutoka katika Halmashauri hizo na kuzitumia katika maeneo yao pamoja na kutumia nyenzo zilizopo kutekeleza operesheni hiyo ili bajeti iliyotengwa na Serikali ikidhi malengo ya operesheni hiyo.

Pia, Mhe. Rais Samia ameelekeza Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwa fedha za mradi huo zielekezwe kwa Wakuu wa Mikoa na kugawanywa kulingana ukubwa wa mikoa husika.

Vile vile, Mhe. Rais Samia ameielekeza Wizara hiyo kufuta kandarasi zote zilizopangwa kwa ajili ya Halmashauri hizo na badala yake ziundwe Kamati maalumu ambazo zitasimamia operesheni hiyo kama zilivyofanya katika ujenzi wa madarasa kupitia fedha za UVIKO 19.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha fedha zilizotengwa kuwezesha Mfumo wa Anuani za Makazi zinatolewa kwa wakati na kuelekezwa kwa Wakuu wa Mikoa ili kufanikisha mfumo huo ikiwa ni pamoja na bajeti ya kujenga mkongo wa mawasiliano katika kila wilaya.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali inafanya jitihada za kuwa na satellite yake itakayoongeza nguvu katika mawasiliano ya mitandao ambayo itawezesha kutunza kumbukumbu za kila mtanzania mwenye anuani ya mtandao.

Vile vile, Mhe. Rais Samia amezielekeza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuzingatia Sheria zinazotaka kuweka majina ya barabara katika barabara zinazojengwa na kuhakikisha kuwa kazi hiyo ni endelevu.

Mhe. Rais Samia ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuendelea kuwashirikisha wananchi na kuwapatia mafunzo katika ngazi za mitaa na vitongoji ili kuhakikisha mradi huo muhimu wa Anwani za Makazi unafanyika na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.  

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu na unapaswa kukamilika mapema ili kuwezesha zoezi muhimu la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti, 2022 kufanyika kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *