TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na wananchi na viongozi mbalimbali katika kukabiliana na mauaji na watu kujiua. 

Rais Samia ametoa agizo hilo wakati akihutubia kwenye Sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya Utumishi wa Askofu Severine Niwemugizi zilizofanyika katika viwanja vya posta, wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Rais Samia amesisitiza kwamba harakati hizo lazima ziwe shirikishi kwani viongozi wa mitaa na vijiji ndio wanaowafahamu watu wao ambao wamekuwa moja ya chanzo cha mauaji hayo.

Takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2020, wilaya ya Ngara pekee kulikuwa na matukio 22 ya mauaji na mwaka 2021 kulikuwa na matukio 21 huku kukiwa na matukio matatu ya watu kujiua mwaka 2020 na mawili mwaka 2021.

Ripoti za uchunguzi huonyesha sababu za ongezeko la matukio ya mauaji na kujiua mara nyingi ni kutokana na wivu wa kimapenzi, kuwania mali, kulipiza visasi, imani za kishirikina, ugomvi wa kifamilia pamoja na msongo wa mawazo.

Rais Samia amesema ameshaliagiza Jeshi la Polisi kufanya utafiti wa kujua sababu za kuongezeka kwa matukio ya mauaji hayo ili kuweza kufanya mikakati ya kupambana na tatizo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *