TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekutana na viongozi wa dini mbalimbali ambapo wamejadili masuala ya maendeleo ya nchi  katika kikao kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa masuala waliozungumzia ni elimu ambapo viongozi hao wamependekeza kuwepo na mjadala mpana kuhusu mfumo mpya utakaokidhi mahitaji ya sasa kwa maana ya kutozalisha jamii ya wahitimu walioandaliwa kuajiriwa peke yake.


Vile vile, wameomba kutotozwa kodi ya mapato kwenye fedha ambazo zinapatikana kama misaada ya hiari ya wanachama na wafadhili kwa ajili ya kuendesha huduma zisizo za kibiashara zikiwemo huduma za wajane na yatima.

Suala la uchafuzi wa mazingira nalo limepewa kipaumbele huku viongozi hao wakitoa wito kwa serikali kuhamasisha upandaji miti ya asili badala ya miti na mbegu kutoka nje ambazo nazo zinahatarisha usalama wa afya za wananchi.

Wakati huo huo, viongozi hao wa dini wametumia mkutano wao na Mhe. Rais Samia kuomba mamlaka husika kutumia busara ili kuangalia namna ya kumaliza kesi inayomkabili kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe  na wenzake.

Ujenzi wa mahusiano bora kwa nchi Jirani na jamii ya kimataifa, fursa za uongozi kwa wanawake na kuulinda Muungano ni baadhi ya mambo aliyopongezwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi hao wa dini.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *