RAIS SAMIA AWATAKA VIONGOZI KUWA WAADILIFU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia Mipango, Sheria, Miongozo, pamoja na Dira ya Maendeleo ya nchi ili kukuza ustawi wa taifa.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo mara baada ya kuwaapisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili pamoja na Wajumbe wake wawili na viongozi wengine pia katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali imedhamiria kukuza uchumi wa nchi baada ya kuathiriwa na UVIKO 19, hivyo ili kufikia azma hiyo ni wajibu kila Kiongozi kwenye kila sekta kutekeleza wajibu na majukumu yake ipasavyo.
Rais Samia amewataka Viongozi hao kusimamia na kutekeleza majukumu waliyopangiwa kikamilifu kwa kushirikiana, kuheshimiana na kuzingatia viapo vyao.
Kwa upande wa Baraza la Maadili, Rais Samia amewataka viongozi aliowaapisha kuanza kazi mara moja kwa kuzifanyia kazi kesi za maadili ndani ya Utumishi wa Umma zinazowasilishwa katika Baraza hilo.
Hafla hiyo ya Uapisho imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Liberata Mulamula, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Katanga pamoja na viongozi wengine wa Serikali.