TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AZINDUA MRADI WA MAJI WA KIGAMBONI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inakwenda kutekeleza ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda mkoani Morogoro litakalotumika kukusanya maji wakati wa mvua.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akizundua miradi ya maji Kigamboni, kukabidhi mitambo ya kuchimba visima na ujenzi wa mabwawa pamoja na kukabidhi eneo la ardhi kwa mkandarasi wa mradi wa bwawa la maji la Kidunda.

Aidha, Rais Samia amesema bwawa hilo lenye thamani ya shilingi bilioni 329 litakalojengwa kwa kutumia fedha za ndani litawezesha kuwepo uhakika wa maji kwa kipindi cha mwaka mzima jijini Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani ambayo kwa sasa yanategemea maji ya Mto Ruvu.

Ujenzi wa bwawa hilo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2022 mpaka 2025 ambapo utakapokamilika utachochea kasi ya maendeleo ya viwanda katika mkoa wa Pwani pamoja na Dar es Salaam.  

Kwa upande mwingine, mradi wa maji wa Kigamboni utaimarisha huduma ya maji katika maeneo ya Temeke, Ilala na Kinondoni hivyo kupunguza ukali wa mgao wa maji.

Hali kadhalika, Rais Samia ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inasambaza maji kwa wananchi katika wilaya ya Kigamboni kwa asilimia 100.

Rais Samia ameitaka Wizara ya Maji kutoa elimu kwa wananchi kuacha kuchoma misitu ovyo, kuchepua maji pamoja na kuingiza mifugo hasa wananchi wanaoishi kando ya vyanzo vya maji kwani  vitendo hivyo husababisha upungufu wa maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *