TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI MANYARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wanasiasa kuacha kuwa kichocheo cha migogoro ya ardhi kwa maslahi yao binafsi.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia wananchi wa Manyara kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kwaraa.

Aidha, Rais Samia amesema wanasiasa wamekuwa na tabia ya kutokuwachukulia hatua wananchi wanaovamia maeneo ya wenzao na badala yake huwatetea na kuwaunga mkono wavamizi hao kwa lengo la kupata kura baadae.

Rais Samia amesema tabia hiyo ya viongozi na wanasiasa inaharibu mipango ya matumizi bora ya ardhi, malengo ya Serikali na kuchelewesha kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

Rais Samia amewataka wanasiasa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kusimamia matumizi bora ya ardhi kwa kila mwananchi na kuwakemea wananchi wanaovamia maeneo ya ardhi ambayo hayakupangwa kwa matumizi hayo.

Rais Samia amekemea tabia ya wakulima na wafugaji kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa kitendo hicho kinahatarisha amani na usalama wa nchi.

Awali, Rais Samia ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Manyara ambayo ilianza kujengwa mwezi Novemba, 2018.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *