TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AWATUNUKU KAMISHENI MAAFISA WANAFUNZI WA JWTZ

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 724 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 03/19 wa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na kundi la 69/21 Refu.

Akitoa maelezo katika sherehe zilizofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Jeshi (TMA) Monduli, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) Brig. Jen. Jackson Mwaseba amesema kati ya wanafunzi waliohitimu wanawake ni 89 na wanaume 635.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete amesema JWTZ imekuwa ikishirikiana na Chuo hicho kutoa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi ambapo kwa kipindi cha miaka 3 ya ushirikiano jumla ya wanafunzi 313 wamehitimu.

Aidha, Dkt. Mwaitete amesema Shahada hiyo inawaandaa maafisa waliohitimu kuweza kuwa mahiri katika kusimamia masuala ya kijeshi, amani pamoja na uongozi kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Dkt. Mwaitete pia amesema Chuo cha Uhasibu kina mpango wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa Shahada mbalimbali zikiwemo usalama wa mitandao, usalama na masomo ya kimkakati, masomo ya ulinzi na amani pamoja na ulinzi wa taarifa

Hali kadhalika, Dkt. Mwaitete amesema Chuo cha Uhasibu kinaunga mkono mpango wa Serikali kupeleka Vyuo vya Elimu ya Juu katika mikoa ya pembezoni kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Pamoja na kutunuku Kamisheni, Mhe. Rais Samia ametoa zawadi kwa Maafisa wanafunzi waliofanya vizuri katika mafunzo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *