TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMEKUSUDIA KULETA MAGEUZI                       YA KILIMO – SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wadau wa kilimo kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wataalam wa kilimo kubuni mipango ya maendeleo  itakayoleta mageuzi katika sekta hii.

Rais Samia ametoa wito huo leo kwenye uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja (block farming); utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji; na kukabidhi mitambo na magari kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliyofanyika Chinangali, wilayani Chamwino.

Aidha, Rais Samia amesema uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana na wanawake kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo bora (Building a Better Tomorrow – BBT).

Vile vile, Rais Samia amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejidhatiti kuhakikisha mpango huu unakuwa endelevu na unafikia mafanikio yaliyokusudiwa.

Rais Samia Pia amesema miongoni mwa malengo ya Serikali kwa upande wa kilimo cha mazao, uvuvi na ufugaji ni kuwa na mchango wa 10% katika pato la taifa mwaka 2030 kutoka 3.6% ya hivi sasa.

Halikadhalika, Rais Samia amemtaka Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kuhakikisha anasimamia kikamilifu fedha zote zinazotolewa katika mradi huo ili iweze kuzalisha bila kufanyiwa ubadhirifu.

Utekelezaji wa Mpango wa Mashamba Makubwa ya Pamoja kupitia BBT umeanzia mkoa wa Dodoma katika Shamba la Chinangali II lenye ekari 400.  Hekta zaidi ya 47,000 zimeshapatikana katika mikoa mingine na upimaji udongo unaendelea ili kutambua mahitaji ya virutubisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *