TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA ATAKA VIKWAZO MPAKANI VIONDOLEWE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara hususan mpakani mwa Tanzania na Malawi ili wananchi waweze kunufaika na biashara zao.

Rais Samia ameyasema hayo kabla ya kuhitimisha ziara yake ya Kiserikali ya siku 3 nchini Malawi, ambapo pia amehudhuria sherehe za miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo.

Kwa pamoja, Rais Samia na Rais wa Malawi Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wamewataka mawaziri husika kukaa chini na kutafakari namna ya kuondoa vikwazo  vya kibiashara ili maono ya Serikali zote mbili yaweze kufikiwa.

Rais Samia pia ameshuhudia utiaji saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Malawi kuhusiana na mashirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Katika mkataba huo, upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye pamoja na Waziri wa Habari na TEHAMA wa Malawi Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa.

Vile vile Rais Samia ameipongeza Malawi kwa kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika shule zake na kusisitiza kwamba lugha hiyo ndio itakayowaunganisha Waafrika.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametembelea eneo la Kapeni view point Blantyre na kujionea athari zilizotokana na kimbunga Freddy ambapo watu wengi walipoteza maisha, mali na makazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *