TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA ASHIRIKI KILELE CHA SHEREHE ZA NANENANE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wakulima kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha na kuuza ziada kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili wapate faida.

Rais Samia ametoa wito huo leo kwenye  kilele cha maonesho ya kilimo na maadhimisho ya sherehe za Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali imedhamiria kuwa na uwezo wa kuhifadhi chakula tani 3,000,000 ifikapo mwaka 2030 ili ziweze kusaidia nyakati za dharura. 

Kwa upande mwingine,  Rais Samia amesema serikali inaendelea kufanya jitihada za makusudi za kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo kwa kuwa kundi hilo ndilo nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Rais Samia pia amesema jitihada hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Programu ya  miaka 8 inayoitwa Building a Better Tomorrow ( BBT) ambapo vijana 812 (wanawake 282 na wanaume 530) wanaendela na awamu ya kwanza ya mafunzo ya kilimo biashara katika vituo atamizi 13. 

Vile vile, Rais Samia amesema juhudi hizi zimeifanya Tanzania kutambulika kimataifa na kuchaguliwa kuwa Mwenyeji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika (African Food Systems Forum) litakalofanyika tarehe 5 -8 Septemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Halikadhalika, Rais Samia amesema Jukwaa hilo litaipatia Tanzania fursa za kibiashara na kuongeza ushirikiano na nchi za Afrika, kwa kuwa na mifumo jumuishi ya kuimarisha kilimo, mifugo na uvuvi itakayochochea zaidi  ajira, uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *