TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito wa kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto ukiwemo mfumo wa kimataifa wa kifedha, unaozuia upatikanaji wa fedha za muda mrefu na za gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo katika nchi zinazoendelea.

Ametaka kuwepo jitihada maradufu na matokeo ya namna ya kushughulikia tofauti za kaskazini-kusini mwa dunia ili kuwa na mkakati thabiti wa kifedha, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi ulio na msingi wa uchumi wa kimataifa.

Rais Samia ameyasema hayo katika kilele cha majadiliano ya mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini (BRICS) uliofanyika jijini Johannesburg.

Katika kipindi hichi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto nyingi, Rais Samia amesema Jumuiya ya Kimataifa lazima iwe moja na iwe tayari kupambana na masuala kama umaskini, tabianchi na upungufu wa chakula.

Mbali na mkutano huo Rais Samia amekutana na viongozi mbalimbali kwa mazungumzo ya mkutano wa BRICS akiwemo Rais wa China Mhe. Xi Xinping, Waziri Mkuu wa Bangladesh Mhe. Sheikh Hasina, Rais Lazarus Chakwera wa Malawi, Rais Macky Sall wa Senegal na Rais Ebrahim Raisi wa Iran.

Katika mazungumzo na viongozi hao baadhi wamekubaliana kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo hususan katika nyanja za biashara, kilimo na ujenzi wa miundombinu.

Rais Samia ameshiriki mkutano huo kwa mwaliko maalum wa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, ambapo nchi za BRICS zimejadili na kuamua kuongeza wanachama wapya 6 wakiwemo Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Argentina, Ethiopia na Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *