TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AFUNGUA MAKAO MAKUU YA PAPU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kuanzisha mfumo wa anuani za makazi na postikodi kama ilivyofanya Tanzania.

Aidha, Rais Samia amesema mfumo huo utarahisisha utoaji wa huduma za kiusalama, afya, fedha, usafirishaji na usambazaji wa vifurushi na mizigo barani Afrika.

Rais Samia ameyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa makao makuu yaUmoja wa Posta Afrika (PAPU) iliyofanyika katika eneo la Phillips.

Rais Samia pia amezitaka Posta za Afrika kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha kufanyika kwa biashara mtandao kwani takriban kila posta imeshaanzisha maduka mtandao kwa ajili ya kuwarahisishia wafanyabiashara shughuli zao.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema jengo hilo litaleta mabadiliko chanya katika kuandaa mikakati ya namna ya kuimarisha huduma za posta kwa nchi wanachama kwenye ukanda wa Afrika ikiwemo ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Vile vile, Rais Samia amesema PAPU italeta mageuzi makubwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ikiwemo kuongeza wigo na ufanisi wa usafirishaji kwa kutumia mashirika ya ndege ya Afrika badala ya kutumia mashirika ya nje.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema serikali imerekebisha Sera ya Taifa ya Posta na kujumuisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na ukuaji wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za posta na kubuni huduma mbadala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *