TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI MKOANI MTWARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuacha kuwanyonya wakulima kwa kuwakata fedha za mauzo na kuzipeleka katika mifuko ya maendeleo ambayo haipo kisheria.

Rais Samia ametoa tamko hilo wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Bomani uliopo Masasi Mji.

Aidha, Rais Samia amewaelekeza viongozi hao kuiweka bayana mifuko iliyopo katika maeneo yao ili ijulikane, ikaguliwe na kuweka wazi mapato na matumizi yake.

Vile vile, Rais Samia amewataka watendaji wa Halmashauri ya Mji wa Masasi kuelekeza fedha za mapato ya halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka serikali kuu.

Kuhusu changamoto ya umeme katika Wilaya hiyo, Rais Samia amesema mkandarasi yuko kazini kuunganisha Masasi na gridi ya taifa na mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 hivyo kufanya umeme kuwa wa uhakika.

Awali Rais Samia alikagua ghala la kuhifadhi chakula la Mangaka wilayani Nanyumbu na kuzungumza na wananchi wa eneo la Round About ambapo amewaeleza kuwa Serikani inatarajia kujenga kongani ya viwanda wilayani humo.

Rais Samia amehitimisha ziara yake mkoani Mtwara na kuanza ziara katika mkoa wa Lindi ambapo amehutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Likongolewe wilaya ya Liwale na Nachingwea mjini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *