TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kutambua umuhimu wa kuchangia huduma za afya kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuwa na uendelevu wa huduma bora.

Rais Samia amesema hayo wakati akizindua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Lumumba ya Mjini Magharibi Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyotokea mwaka 1964.

Rais Samia amesema wananchi wanapaswa kuwa na Bima ya Afya ili waweze kupata huduma bora za matibabu zinazolingana na uwekezaji wa miundombinu inayojengwa.

Rais Samia amewakumbusha watumishi na wagonjwa watakaotumia hospitali hiyo na vifaa vyake kuvitunza ili vidumu.  

Aidha Rais Samia ameitaka Wizara ya Afya kuhakikisha hospitali hiyo inabaki hivyo hivyo kama inavyokabidhiwa kwao pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kupata matokeo chanya.

Rais Samia pia amewataka madaktari na wauguzi kufanya kazi zao kwa weledi na kujali wagonjwa wakiwemo wajawazito wanaofika kujifungua.

Fedha zilizotumika kujenga na kununua vifaa tiba ni mkopo nafuu wa Bilioni 29 kutoka Shirika la Fedha Duniani-IMF kwa ajili ya kuimarisha mazingira na kukabiliana na Uviko 19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *