Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea maua kutoka kwa watoto leo muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe ambapo atashiriki katika mkutano wa 34 wa siku mbili wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC Agosti 17,2014.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe Agosti 17,2014.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia na Rais Jackob Zuma wa Afrika ya kusini wakijadiliana jambo kabla ya kuanza kwa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika hoteli ya Elephant Hills, mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe Agosti 18,2014.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wakuu na wawakilishi wa nchi za Jumuiya ya uchumi kusini mwa Afrika SADC muda mfupi baada ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa jumuiya hiyo uliofanyika katika hoteli ya Elephant Hills mjini Victoria Falls Zimbabwe leo.Katikati ni mwenyeji wa Mkutano huo Rais Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe Agosti 17,2014
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais Robert Gabriel Mugabe Rais wa Zimbabwe akimkabidhi Bi. Sheila Hashim Mbita, binti yake Brigedia Jenerali Mstaafu Hashim Mbita Tuzo ya Juu ya Taifa la Zimbabwe ya Nishani ya Royal Order Of Mwanamutapa kwa kutambua mchango wake katika ukombozi wa Taifa la Zimbabwe na nchi nyingine kusini mwa Afrika.Rais Mugabe alikabidhi tuzo hiyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe Agosti 17,2014
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha nne Neema Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari Naboti Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utunzi wa insha katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya uchumi ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe ambapo mwanafunzi huyo aliandika insha inayohusu mabadiliko ya tabia nchi. Agosti 17,2014
- MSICHANA WA KITANZANIA ASHINDA MASHINDANO YA INSHA YA SADCNi Neema Steven kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Njombe
- Awabwaga washindani 39 wa kanda mbali na wa nyumbani
Mtoto wa Kitanzania,msichana Neema Steven Mtwanga, ameibuka kinara katika Mashindano ya Utunzi wa Insha katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa washindani 39 waliowania Tuzo ya Utunzi wa Insha hiyo kwa Mwaka 2014.
Msichana Neema Steven Mtwanga, 16, kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Mkoa wa Njombe, ametunukiwa Tuzo ya ushindi huo katika Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC ulioanza leo katika Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe.
Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe na nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland.
Kwa ushindi huo, Neema Steven Mtwanga ambaye yuko kidato cha nne, amezawadiwa hundi ya dola za Marekani 1500 ambayo ni sawa na shilingi milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kumwezesha kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC na kukabidhiwa zawadi hiyo. Aidha, Neema amepewa zawadi ya ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya mawasiliano na habari.
Mashindano hayo ya Insha ya Mwaka 2014 yalianzishwa rasmi Oktoba, 2013 ambako washindani walitakiwa kuandika Insha kuhusu mada: “Climate Change is having adverse effect on the socio-economic development in the Region. What should the Education Sector do to mitigate the impact on the youth” – Mabadiliko ya Tabia Nchi yanaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kanda ya SADC. Nini Sekta ya Elimu ifanye kupunguza athari hizo kwa vijana?
Insha 39 zilipokelewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC ikiwa ni Insha tatu kwa kila nchi. Insha zilipokelewa kutoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa Insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, Julai, mwaka huu kupitia Insha zote na kutoa uamuzi wa nani washindi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa SADC umepokea kwa furaha ushindi wa msichana Neema ukieleza kuwa ushindi huo umeiletea Tanzania heshima kubwa katika eneo la SADC na nje ya eneo hilo.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Rais Jackob Zuma wa Afrika ya Kusini pamoja na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) wakati wa dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kwa ajili ya viongozi wa SADC wanaohudhuria mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe