Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kwa masikitiko makubwa ametangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,
Mhe. Benjamin William Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 24 Julai,
2020.
Mhe. Rais Magufuli amesema Mhe. Benjamin William Mkapa amefariki dunia
hospitalini Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na wastahimilivu
baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Mhe. Benjamin
William Mkapa.
“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin
William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia, amefariki
dunia katika hospitali Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe
Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea
Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele za
haki, taarifa zingine zitaendelea kutolewa lakini Mzee Mkapa hatuanaye tena”
amesema Mhe. Rais Magufuli katika taarifa yake kwa Taifa.
Taarifa zingine kuhusiana na msiba huu mkubwa zitatolewa baadaye.
Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ametangaza siku 7 za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa tarehe 24
Julai, 2020 kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin
William Mkapa kilichotokea Jijini Dar es Salaam.
Katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Watanzania wote kuendelea kuwa watulivu,
wastahimilivu na wamoja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya
kuondokewa na mpendwa wao, Rais Mstaafu Mkapa.