Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Oktoba, 2020 amekutana na familia ya kijana Briton Wilfred Mollel (26) aliyeuawa kikatili tarehe 25 Agosti, 2020 baada ya kushambuliwa katika vurugu zilizotokea wakati wa urejeshaji wa fomu za kugombea udiwani kwa msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Kaloleni katika Jimbo la Tunduma Mkoani Songwe.
Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mama wa Marehemu aitwaye Roda Bryson Mwaisongole na Mjane wa Marehemu aitwaye Salome Philemon Mayao Mjini Tunduma ambapo amewapa pole na kutoa ubani wa shilingi Milioni 6.
Marehemu Briton Wilfred Mollel aliyekuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alimsindikiza mgombea udiwani wa CCM katika kata ya Kaloleni wakati wa urejeshaji wa fomu siku ya tukio.
Mhe. Rais Magufuli amelaani mauaji hayo na ameagiza hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika.
Mhe. Rais Magufuli na wanafamilia hao wamefanya sala fupi ya kumuombea Marehemu apumzike kwa amani, Amina.
Marehemu Briton Wilfred Mollel ameacha Mke na watoto 3 wenye umri wa kati ya mwaka 1 na miaka 6.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ambaye amewasili Mjini Unguja (Zanzibar) amemtembelea na kumjulia hali Bw. Hamis Nyange Makame (63) aliyelazwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja akitibiwa majeraha baada ya kushambuliwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni wakati akiswali Msikitini huko Kangagani, Wilaya ya Wete (Pemba).
Bw. Hamis Nyange Makame (Prof. Gogo) ambaye ni mwanachama wa CCM alishambuliwa tarehe 22 Septemba, 2020.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na shambulio hilo la kikatili na ameviagiza vyombo vya dola kuchukua hatua zinazostahili kwa wote waliohusika.
HABARI PICHA :
Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimfariji
Ndugu Hamisi Nyange Makame maarufu kama Profesa Gogo (63) aliyekatwa mapanga na wenzie wawili wakati wa Swala ya Alfajiri katika msikiti wa eneo la Kangagani wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini. Rais Magufuli alimtembelea majeruhi huyo katika hospitali ya Mnazi Mmoja alikolazwa mara tu baada ya kuwasili akitokea Songwe tayari kwa mikutano ya kampeni ya Chama cha Mapinduzi visiwani Zanzibar leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na kuwapa pole Familia ya Marehemu Briton Wilfred Mollel (26) Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM aliyeuwawa tarehe 25 Agosti 2020 Tunduma mkoani Songwe, kulia ni Mama Mzazi wa Marehemu Roda Bryson Mwaisongole akiwa pamoja na mke wa Marehemu Salome Philemon Mayao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ame wakabidhi rambirambi yake ya Sh. Milioni 3 kwa Mama Mzazi wa Marehemu Briton Wilfred Mollel, Roda Bryson Mwaisongole na Sh.milioni 3 nyingine kwa mjane wa marehemu ili ziwasaidie katika kipindi hiki kigumu.