RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AFUNGUA VIWANDA VITATU MKOANI MOROGORO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 12 Februari, 2021 amezindua viwanda vikubwa 3 vilivyopo Mkoani Morogoro na ameagiza viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uwekezaji na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuondoa urasimu unaokwamisha ujenzi wa viwanda hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli aliyekuwa katika ziara ya kikazi ya siku 2 Mkoani Morogoro, kwanza amezindua kiwanda cha ngozi Taifa (Taifa Leather Company Limited) kilichowekezwa na Mtanzania Bw. Rostam Aziz kwa gharama ya takribani shilingi Bilioni 50.

Kiwanda hicho kikubwa zaidi Barani Afrika kina uwezo wa kuchakata vipande 4,000 vya ngozi ya wanyama wakubwa na vipande 10,000 vya ngozi ya wanyama wadogo kwa siku na kinatarajiwa kuongeza uzalishaji mwishoni mwa mwaka 2022 ambapo kitachakata vipande 5,000 vya ngozi ya wanyama wakubwa na vipande 15,000 vya ngozi za wanyama wadogo.

Baada ya kuzindua kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Rostam Aziz kwa uwekezaji huo, ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanyia kazi maombi ya kuondoa kodi katika kemikali za kuchakatia ngozi na ameagiza kuongezwa kwa kiwango cha kodi kutoka asilimia 80 hadi 100 kwa ngozi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi zikiwa ghafi ili ngozi hizo ziweze kuchakatwa hapahapa nchini ambapo zitaongeza ajira na mapato ya Serikali.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa na watu waliobinafsishiwa viwanda na kisha kutoviendeleza akiwemo Mhe. Aziz Abood aliyebinafsishiwa viwanda vya mafuta ya mgando (Moproco Factory) na maturubai (Morogoro Canvas) na ameagiza Benki ya CRDB na Msajili wa Hazina kuhakikisha viwanda hivyo vinagawiwa kwa wawekezaji wengine mara moja baada ya Mhe. Aziz Abood kunyang’anywa.

Pili, Mhe. Rais Magufuli amezindua kiwanda kukoboa mpunga (Murzar Wilmar Rice Mills Ltd) kilichojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 48 na ambacho kina uwezo wa kukoboa tani 288 za mpunga kwa siku na kisha kufungasha mchele katika ujazo na madaraja mbalimbali.

Kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 75 na kinanunua mpunga kutoka kwa wakulima takribani 5,000 kutoka Mikoa ya Morogoro, Mbeya, Shinyanga na Tabora ambapo katika mwaka 2020 kimenunua tani 65,000 zenye thamani ya shilingi Bilioni 45.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Murzar Wilmar Rice Mills Ltd kwa kuwekeza katika kiwanda hicho kikubwa kuliko vyote hapa nchini kwa kukoboa mpunga, ametoa wito wamiliki wake kuutambulisha mchele unaozalishwa kiwandani hapo kwa majina ya Kitanzania badala ya jina linalotumika sasa na pia ameeleza kutofurahishwa na nchi kuendelea kuuza nje ya nchi mazao ambayo hayajasindikwa na kuongezwa thamani mfano mpunga badala ya mchele na mahindi badala ya unga.

Tatu, Mhe. Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kusafisha na kufungasha mazao ya jamii ya kunde (Choroko, mbaazi, dengu, pilipili manga, karafuu, ufuta, maharage na karanga) kilichojengwa na kampuni ya Mahashree Agro Processing Tanzania Limited katika eneo la Mikese kwa gharama ya shilingi Bilioni 25.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni hiyo kwa kuwekeza katika kiwanda ambacho kitawawezesha wakulima wa mazao hayo kupata soko na ametoa wito kwa wawekezaji wengine wa ndani na nje ya Tanzania kuja kuwekeza hapa nchini kwa kuwa wawekezapo hapa watakuwa na uhakika wa soko la watu takribani Milioni 60 wa Tanzania, watu takribani Milioni 165 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na watu takribani Milioni 400 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADS), ambazo zina makubaliano ya kuondoa vikwazo na kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano wa biashara na uwekezaji.

Mhe. Rais Magufuli ameikaribisha kampuni ya Mahashree Agro Processing Tanzania Limited kuwekeza katika uzalishaji wa sukari kama ilivyoahidi na ametaka viongozi wanaohusika kuwezesha mpango huo kwa kuwa wazalishaji wa sukari hapa nchini hawajaongeza uzalishaji kama walivyoahidi.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamis Taletale (Babu Tale) la kujengwa barabara ya lami ya Bigwa – Kisaki (km 78) ambapo ameiagiza Wizara ya ujenzi na uchukuzi kutangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa kilometa 40 za mwanzo kwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi na ustawi wa wananchi wa Morogoro Kusini.

Mhe. Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya siku 2 Mkoani Morogoro na ameingia Mkoani Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *