TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Februari, 2021 amefungua daraja la juu katika makutano ya barabara ya Morogoro, Mandela na Sam Nujoma (Ubungo) na amefungua Kituo cha Mabasi cha Kimataifa kilichopo Mbezi Luis Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya ufunguzi wa daraja la juu la Ubungo imefanyika kando ya barabara hizo ambapo Mhe. Rais Magufuli ameamua daraja hilo liitwe Daraja la Kijazi (Kijazi Interchange) ikiwa ni kutambua utumishi uliotukuka wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Marehemu Balozi Mhandisi John William Kijazi (aliyefariki dunia tarehe 17 Februari, 2021) katika maendeleo ya nchi.

Daraja la Juu la Kijazi lina barabara za chini zinazoelekea pande 4 za makutano, lina barabara ya juu ya kwanza inayoiunganisha barabara ya Morogoro moja kwa moja bila kusimama na lina barabara ya juu ya pili inayoziunganisha barabara za Sam Nujoma na Mandela moja kwa moja bila kusimama. Barabara zote zina njia 6 zikiwemo njia 2 za mabasi yaendayo haraka (BRT).

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo uliochukua muda wa miezi 30 umegharimu shilingi Bilioni 252.622 na kwamba daraja hilo lenye uhai wa zaidi ya miaka 100 limetatua changamoto ya msongamano wa magari takribani 68,880 kwa siku ambayo hupita katika makutano hayo.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kwa kuwa litaondoa adha iliyowakumba wananchi wa Dar es Salaam na wageni wanaoingia katika Jiji hilo ambao walijikuta wakipoteza muda mwingi wa kufika ama kutekeleza majukumu yao na wengine kupoteza maisha wakiwa wanawahi hospitali kwa matibabu.

Amewahakikishia wananchi wa Dar es Salaam kuwa dhamira yake ya kuliboresha Jiji hilo ipo palepale na kwamba baada ya kazi nzuri ya kuzijenga barabara kuu, Serikali itajielekeza kujenga barabara za mitaani kwa kiwango cha lami, kujenga barabara za juu katika makutano 10 ya barabara na kuimarisha huduma nyingine za kijamii.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema anakusudia kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na badala yake Halmashauri mojawapo ya Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam itapandishwa hadhi na kuwa Jiji ili kuondoa hali ya sasa ambapo kuna Halmashauri ya Jiji inayotumia maeneo ya utawala ya Halmashauri za Manispaa.

Baada ya kufungua Daraja la Juu la Kijazi, Mhe. Rais Magufuli amefungua Kituo cha Mabasi cha Kimataifa kilichopo Mbezi Luis Jijini Dar es Salaam na ameridhia ombi la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo la kituo hicho kuitwa Kituo cha Mabasi cha Kimataifa Magufuli kutokana na kutambua mchango wake katika uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla.

Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli ambaye awali alikuwa anasita kukubali kituo hicho kuitwa jina lake, amekubaliana na ombi Waziri Jafo kwa sharti kuwa hataki kituo hicho kitumike kuwanyanyasa baadhi ya Watanzania hasa wa hali ya chini na hivyo ameitaka TAMISEMI na Jiji la Dar es Salaam wahakikishe wafanyabiashara wadogo (Machinga) na Mama Lishe wanaruhusiwa na wanapatiwa maeneo ya kufanya biashara zao badala ya kituo chote kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa pekee.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuridhishwa kwake na matumizi ya shilingi Bilioni 50.95 zilizotumika kujenga kituo hicho na ametaka miundombinu ya kituo hicho itunzwe vizuri ili idumu kwa muda mrefu.

Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema majengo ya kituo hicho yenye ghorofa 4 kwenda juu na 2 kwenda chini yamezungukwa na maeneo ya kuegesha mabasi 358 kwa wakati mmoja na magari madogo  280, na kwamba kituo hicho chenye maeneo ya huduma za kijamii kitazalisha mapato ya shilingi Bilioni 10.2 kwa mwaka, ajira 10,000 na kupunguza msongamano wa magari ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Wabunge wa Ubungo (Mhe. Prof. Kitila Mkumbo) na Kibamba (Mhe. Issa Mtemvu) kwa jinsi wanavyowapigania wananchi wao ambapo pamoja na kukubali kutengeneza barabara za lami za mitaa ya majimbo hayo na kuimarisha zaidi huduma za maji, amekubali ombi la kupatiwa eneo la pori la ekari 52 lililokuwa chini ya Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kujenga miundombinu ya huduma za kijamii za wananchi wa Kibamba.

Mhe. Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake hapa Jijini Dar es Salaam ambapo ataweka jiwe la msingi la soko la kisasa la Kisutu, atazindua jengo la Jitegemee na uzinduzi wa studio za Channel Ten, Channel Ten Plus, Redio Magic FM na Redio Classic FM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *