TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 19 Machi, 2021 ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hafla ya kuapishwa kwake imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo pia amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Mhe. Rais Samia ameshika wadhifa huo baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufariki dunia tarehe 17 Machi, 2021 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kula kiapo, Mhe. Rais Samia ametoa salamu za pole kwa Mjane wa Marehemu Mama Janeth Magufuli, Mama wa Marehemu Mama Suzan Magufuli, wanafamilia na Watanzania wote kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Mhe. Rais Samia amesema Mhe. Dkt. Magufuli alikuwa na kiu, nia na dhamira ya dhati ya kutaka kuibadili Tanzania kwa mafanikio zaidi na kwamba Watanzania wote ni mashahidi kwa namna alivyofanikiwa kuibadili taswira ya nchi kwa utendaji wake imara usiotikisika huku akimtanguliza Mungu.

“Sote tulisikia matamanio na maono yake makubwa kwa nchi hii aliyoyatafsiri katika mipango mikakati na ujenzi wa miradi mikubwa, mimi nilipata bahati ya kuwa makamu wake, alikuwa ni kiongozi asiyechoka kufundisha, kuelekeza kwa vitendo vile anataka nchi iwe au nini kifanyike, amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha, naweza kusema bila chembe ya shaka kuwa tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwanamwema wa Bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli” amesema Mhe. Rais Samia.

Amewataka Watanzania wote kujenga umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu na amewahakikishia kuwa Taifa lipo imara na viongozi wamejipanga vizuri kuendeleza pale alipoishia Mhe. Dkt. Magufuli.

Mhe. Rais Samia ametangaza siku 21 za maombolezo ya Kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti na amesisitiza kuwa “Katika kipindi hiki cha maombolezo, huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, udugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na Utanzania wetu, huu sio wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini, si wakati wa kutazama yaliyopita bali kutazama yajayo, sio wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana ili tuweke nguvu zetu za pamoja kujenga Tanzania mpya ambayo mpendwa wetu Rais Magufuli aliitamani”.

Mhe. Rais Samia amesema mwili wa Dkt. John Pombe Magufuli utazikwa tarehe 25 Machi, 2021 nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *