MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWAAPISHA KATIBU MKUU KIONGOZI MAWAZIRI , NA MANAIBU WAZIRI ALIO WATEUA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 01 aprili, 2021 amemuapisha Mhe. Balozi Hussein Athman Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na amewaapisha Mawaziri 8 na Naibu Mawaziri 8 aliowateua jana.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.

Katibu Mkuu Kiongozi aliyeapishwa ni Mhe. Balozi Hussein Athman Kattanga.

Mawaziri walioapishwa ni Mhe. Ummy Ally Mwalimu (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI), Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Waziri wa Katiba na Sheria), Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Waziri wa Fedha na Mipango) na Mhe. Selemani Saidi Jafo (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira). 

Mawaziri wengine walioapishwa ni Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Waziri wa Viwanda na Biashara), Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji), Mhe. Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora).

Naibu Mawaziri walioapishwa ni Mhe. William Tate Ole Nasha (Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji), Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi), Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara (Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi) na Mhe. Pauline Philipo Gekul (Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo).

Naibu Mawaziri wengine walioapishwa ni Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Naibu Waziri wa Fedha na Mipango), Mhe. Mbarouk Nassoro Mbarouk (Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Mhe. Mwanaidi Ally Hamis (Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) na Mhe. Hamad Hassan Chande (Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira).

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Samia amemtaka Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Katanga kusimamia ipasavyo jukumu la kuratibu vizuri shughuli za wizara, taasisi na idara za Serikali ili kuondoa changamoto ya kila moja kufanya kazi kivyake, na amesisitiza kuwa hakuna sababu ya Wizara, taasisi na idara hizo kuvutana kwa kuwa zote zinatumikia Serikali moja.

Kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Mhe. Rais Samia amesema amefanya uteuzi na mabadiliko hayo kwa kumpeleka kila Waziri katika eneo alilobobea kitaaluma au kiuzoefu na pia kwa kuzingatia Muungano.

Amewataka kuchapakazi kwa juhudi na maarifa huku akiwataka wale wote ambao wameanza harakati za kugombea nafasi za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuacha mara moja kwani atawatupia macho kwa ukaribu na kuwapima kwa matokeo ya majukumu waliyokabidhiwa.

Mhe. Rais Samia amemuagiza Mhe. Mwigulu Nchemba kutekeleza lengo la kufikia makusanyo ya wastani wa shilingi Trilioni 2 kwa mwezi ifikapo mwisho wa mwaka huu kwa kuongeza akili na maarifa ya ukusanyaji kodi ikiwemo kupanua uwigo wa kodi, badala ya kutumia nguvu kwa kunyang’anya vifaa vya biashara, kufungia akaunti za benki na kuchukua pesa kwa nguvu mambo ambayo yanaua biashara na kusababisha wafanyabiashara kuhamishia biashara zao nchi jirani.

Mapema katika salamu zake Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewaagiza Mhe. Waziri Mwigulu na Mhe. Waziri Jafo kuanza kazi kwa kushughulikia suala la ushirikiano wa kifedha ndani ya Muungano na amekemea tabia za mivutano kati Mawaziri na Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *