Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 18 Aprili, 2021 amehudhuria kongamano la viongozi wa Dini lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa maisha ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kuliombea Taifa.
Pamoja na Mhe. Rais Samia, kongamano hilo limehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Philip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samwel Malecela, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Athman Kattanga, Mawaziri, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Katika kongamano hilo, viongozi wakuu kutoka madhehebu mbalimbali ya Dini wamemuombea Dua Hayati Dkt. Magufuli, wamewaombea Dua Mhe. Rais Samia na Mhe. Rais Mwinyi na wametoa mada kuhusu umuhimu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo, utiifu, namna bora ya kumuenzi Hayati Dkt. Magufuli, wajibu wa wananchi kuwaombea viongozi, mafunzo aliyotuachia Hayati Dkt. Magufuli pamoja na umoja na mshikamano.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuandaa kongamano hilo na kwa kuungana nae katika kipindi kigumu cha maombolezo na maziko ya Hayati Dkt. Magufuli na amewahakikishia viongozi hao kuwa anatambua mchango wa Dkt. Magufuli kwa jinsi alivyowathamini na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za Serikali kiuchumi na kijamii na kwamba utamaduni huo atauendeleza.
Ametoa wito kwa viongozi wa Dini kuendelea kuwaongoza Watanzania kuliombea Taifa na amewakumbusha Waumini wa Dini ya Kiislamu kuwa kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni cha rehema, toba, na maghufira hivyo wakitumie kujiweka karibu zaidi na Allah (S.WT).
Mhe. Rais Samia amefafanua kuwa uongozi wake wa Awamu ya Sita haukutokana na uchaguzi, bali umetokana na Awamu ya Tano hivyo amesema “mwelekeo wa Awamu ya Sita utakuwa ni kudumisha mema yaliyopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mema mapya, ndio maana halisi ya kaulimbiu yangu ya Kazi Iendelee”.
Aidha, ametaja vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita ambavyo ni kuendeleza tunu za Taifa ambazo ni kudumisha amani, umoja, mshikamano, uhuru wa Nchi na mipaka yake, kulinda Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Vipaumbele vingine ni kuendeleza jitihada za kukuza uchumi mkuu na kuutafsiri katika uchumi wa watu, kupambana na rushwa, uhujumu uchumi, wizi, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha misingi ya utoaji haki, usawa, uhuru na demokrasia na kukamilisha miradi ya kimkakati na kielelezo yote pamoja na kuangalia uwezekano wa kuibua miradi mipya.
Pia, Serikali itaboresha mazingira ya biashara, kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali, kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia mitaji kutoka nje na kuendelea kukuza uhusiano wa Kimataifa.
Mhe. Rais Samia ameelezea kutofurahishwa kwake na mijadala ya mitandaoni inayomlinganisha yeye na Hayati Dkt. Magufuli na ambayo Waheshimiwa Wabunge wameichukua na kuizungumza Bungeni, hivyo amewasihi Wabunge kujikita katika mijadala ya msingi inayohusu Bunge la Bajeti linaloendelea na vikao vyake hivi sasa.
Kuhusu janga la Korona (Covid-19), Mhe. Rais Samia amesema tayari ameshaunda kamati ya wataalamu ya kumshauri kuhusu ugonjwa huo na wakati kamati hiyo ikiendelea amewaomba viongozi wa Dini wawasihi waumini wao kuendelea kuzingatia tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu juu ya kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Mwinyi amewapongeza viongozi wa Dini kwa kuandaa kongamano hilo na amewasihi Watanzania wote kuzingatia mafundisho aliyoyaacha Hayati Dkt. Magufuli na kumuunga mkono Mhe. Rais Samia ambaye ana dhamira ya dhati ya kuendeleza mazuri yote aliyoyaanzisha Hayati Dkt. Magufuli.
Mwakilishi wa familia ya Hayati Dkt. Magufuli ambaye ni mwanae Bw. Joseph Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Samia, viongozi mbalimbali na Watanzania wote kwa jinsi walivyowafariji na kuungana nao katika kipindi kigumu cha maombolezo na kwa kudumisha amani.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Leave a reply