RAIS FILIPE JOCANTO NYUSI WA MSUMBIJI AFANYA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU MOJA NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji na Mwenyekiti wa SADC Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakipunga mkono kuwaaga wananchi waliojitokeza wakati wa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda -Chato mkoani Geita

Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi leo tarehe 11 Januari, 2021 amefanya ziara ya kikazi ya siku 1 hapa nchini ambapo amekutana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Geita uliopo Chato, Mhe. Rais Nyusi amepokewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na kisha viongozi hao wakaelekea katika eneo la Kitela ambako wameweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewaeleza Waheshimiwa Marais kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali hiyo imefikia asilimia 90 kwa gharama ya shilingi Bilioni 16 na kwamba hospitali nyingine kama hiyo inajengwa katika Kanda ya Kusini huko Mkoani Mtwara.


Dkt.Gwajima ameeleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuimarisha huduma za matibabu yakiwemo matibabu ya kibingwa na kwamba pamoja na kujengwa kwa hospitali za kanda, Serikali imejenga Hospitali mpya 5 za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya 99, Vituo vya Afya 487 na Zahanati 1,198 nchi nzima.


Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia wananchi takribani milioni 14 kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria na Mikoa ya Kanda ya Magharibi.
Akizungumza na wananchi waliohudhuri sherehe za uwekaji jiwe la msingi la hospitali hiyo, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nyusi kwa kukubali kuweka jiwe hilo la msingi na ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha awamu zilizobaki za ujenzi wa hospitali hiyo zinaunganishwa na kufanya kwa pamoja ili ikamilike haraka na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.


Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa kujengwa kwa hospitali hiyo ni muendelezo wa kazi nzuri ya ujenzi wa Wilaya ya Chato iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alitembelea Chato tarehe 09 Januari, 1967 ambapo alifungua kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato (Chato Ginnery) chenye uwezo wa kuchambua marobota 20,000 ya pamba kwa mwaka na akaanzisha mchango wa ujenzi wa Bandari ya Nyamirembe iliyopo Chato kwa ajili ya kusafirisha pamba kwenda Mwanza na kwingineko. Yeye mwenyewe Hayati Mwl. Nyerere alichangia paundi 1,000 sawa na shilingi 20,000 (kwa wakati huo).
Ameongeza kuwa kitendo cha Hayati Mwl. Nyerere kuanzisha mchango wa kujenga Bandari ya Nyamirembe, kiliitikiwa na wananchi na hatimaye kukamilisha bandari hiyo kwa gharama ya paundi 10,000 na kwamba ujenzi huo ulifanikiwa kutokana na kuhimiza dhana ya kujitegemea. Siku chache baadaye yaani tarehe 05 Februari, 1967 Hayati Mwl. Nyerere alikwenda Arusha ambako alitangaza Azimio la Arusha ambalo pia lilikuwa linahimiza kujitegemea.


Ameongeza kuwa juhudi hizo ziliendelezwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi aliyeitembelea Chato wakati wa kipindi chake, Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamini William Mkapa aliyeitangaza Chato kuwa Wilaya mpya ikitokea Wilaya ya Biharamulo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyeizindua Wilaya ya Chato.


Kwa upande wake, Mhe. Rais Nyusi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumpa heshima ya kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa za kuwajali watu kwa kujenga sehemu za huduma za matibabu na kujenga miundombinu mingine mbalimbali ambayo inawahudumia wananchi na kukuza uchumi.
Mhe. Rais Nyusi ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli kwa kuchapa kazi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewajalia nchi yenye rasilimali na utajiri mkubwa.
Baada ya kuweka jiwe la msingi la hospitali hiyo, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Nyusi wamefanya mazungumzo na baadaye kuzungumza na Vyombo vya Habari ambapo wamesema ziara hii imefanyika kwa lengo la kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania na Msumbiji ni ndugu, marafiki na majirani wa kweli.
Mhe. Rais Nyusi amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 1 na amerejea nchini Msumbiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *