TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 09 Desemba, 2021 ameongoza watanzania katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizofanyika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Katika Sherehe hizo, Mhe. Rais Samia amekagua gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana na vikundi vya Ulinzi na usalama. Pia alipokea  salamu za utii, kisha gwaride hilo kupita kwa heshima mbele yake kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka.

Aidha, katika sherehe hizo JWTZ lilionyesha baadhi ya zana vita zinazotumika katika medani za vita pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa mgeni rasmi, Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame, Rais wa Msumbiji Mhe. Philepe Nyusi, Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Azali Assoumani, wawakilishi wa Viongozi kutoka nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Oman na Uswatini pamoja na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Katika hatua nyingine, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametunuku Nishani 14 ikiwa ni sehemu ya Nishani 893 alizozitunuku kwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini.

Waliotunukiwa Nishani ya Miaka 60 ya Uhuru ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Simon Nyakoro Sirro, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Kamishna Diwani Athumani Msuya, Mkuu wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kamishna Jenerali John William Masunga na Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji Kamishna Jenerali Dkt. Anna Peter Makakala.

Waliotunukiwa Nishani ya Utumishi Uliotukuka ni Meja Jenerali Hawa Issa Kodi, Kamishna wa Polisi Shaban Mrai Hiki na Kamishna Msaidizi wa Magereza Mkwanda Hasseid Mkwanda.

Vile vile, Afisa Mteule Daraja la I Martin Peter Kazilo kutoka JWTZ, Mkaguzi wa Polisi Stahmil Herman Lusatila, Mkaguzi wa Magereza Nicerosiana Elisa Malisa, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Ishima Shomari Seif na Mkaguzi wa Idara ya Uhamiaji Abubakary Muhonzi Yunusu walitunukiwa Nishani ya Utumishi Mrefu na Tabia Njema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *