Daily Archives: July 16, 2020

Taarifa kwa vyombo vya Habari

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Julai, 2020 amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.
Viongozi hao ni Bw. Aboubakar Kunenge aliyeapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Joseph Joseph Mkirikiti aliyeapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bw. Paulo Mshimo Makanza aliyeapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gabriel Pascal Malata aliyeapishwa kuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniface Nalija Luhende aliyeapishwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Maduhu Isaac Kazi aliyeapishwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia Wakuu wa Mikoa wakiwaapisha Wakuu wa Wilaya ambapo Kanali Patrick Norbert Songea ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto (Manyara), Ghaibu Buller Lingo ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang (Manyara), Alhaji Mwangi Rajab Kundya ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi (Kilimanjaro), Mayeka Simon Mayeka ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya (Mbeya) na Dkt. Seleman Hassan Serera ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa (Dodoma).
Viongozi hao pamoja na viongozi wengine ambao ni Bw. Joseph Kashushura Lwiza aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu (Kigoma), Bw. Frank Fabian Chonya aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa (Lindi), Bw. Juvenile Jaka Mwambi aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tandahimba (Mtwara), Bw. Mashaka Boniface Mgeta aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni (Tanga), Bi. Johari Khamis Athman aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Rombo (Kilimanjaro) na Bw. Ayub Amir Perro aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa (Lindi) wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa Umma.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka kwenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kutatua kero zinazowakabili ikiwemo migogoro mbalimbali ambayo inakwamisha juhudi za maendeleo ya wananchi hao.
Mhe. Rais Magufuli amewasihi viongozi wa Serikali kuridhika na nyadhifa walizonazo na kuelekeza nguvu zao kulitumikia Taifa badala ya kung’ang’ania kutaka nafasi zingine.
Amemtaka Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Pascal Malata na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Nalija Luhende kuhakikisha wanasimamia vizuri kesi zinazoihusu Serikali ili kulinda maslahi ya Taifa.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Isaac Kazi kuhakikisha TIC inavutia wawekezaji zaidi na inaondoa vikwazo dhidi ya wawekezaji wenye nia ya kuwekeza hapa nchini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jafo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa.

 

Mhe. Rais awaapisha viongozi mbalimbali Ikulu ya Chamwino Dodoma

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na viongozi mbalimbali katika hafla fupi ya Uapisho wa Viongozi hao iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 16 Julai 2020.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiondoka katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma mara baada ya hafla fupi ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali aliowateua.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw. Aboubakar Kunenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 16 Julai 2020.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Gabriel Pascal Luhende kuwa Wakili Mkuu wa Serikali katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 16 Julai 2020.