Daily Archives: January 29, 2016

RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AWATEUA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA YA MWANZA NA KATAVI

276a85f3-9d16-4ddb-85d2-eb7b4be3920f

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akizungumza na wanahabari hawapo pichani kuhusu uteuzi wa Makatibu Tawala wa Mikoa ya Mwanza na Katavi ambao wameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Januari 29,2016 Ikulu jijini Dar es Salaam

 

HABARI KAMILI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wawili wa mikoa ya Mwanza na Katavi ili kujaza nafasi za Makatibu Tawala wa mikoa hiyo.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema Rais amemteua Kamishna wa Polisi, Clodwing Mtweve kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, ambako anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Faisal Issa ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Kabla ya Uteuzi huo, Kamishna Mtweve alikuwa Kamishna wa fedha na Utawala wa Jeshi la Polisi Tanzania.

Balozi Sefue amesema Rais Magufuli pia amemteua Kamishna wa polisi Paul Chagonja kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi ambako anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Madeni Kipande ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Kabla ya Uteuzi huo, Kamishna Chagonja alikuwa Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi Tanzania.

Aidha, Balozi Ombeni Sefue amesema Rais Magufuli ameamua kuwateua Makamishna hawa wa Polisi kama alivyowateua Majenerali wa Jeshi la Wananchi Tanzania kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, kwa lengo la kujenga nidhamu katika utumishi wa umma.

Makamishna Clodwing Mtweve na Paul Chagonja pamoja na Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim ambaye ameteuliwa kuwa Balozi Mpya wa Kuwait, wataapishwa kesho Jumamosi tarehe 30 Januari, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, saa nne asubuhi.

 

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam.

29 Januari, 2016