RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN ASHUHUDIA MAKAMU WA RAIS AKIAPA IKULU YA CHAMWINO MKOANI DODOMA.

Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 31 Machi, 2021 ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Dkt. Mpango ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Mawaziri na Naibu Mawaziri na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Wengine ni Mawaziri Wakuu wastaafu (Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda), Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Philip Mangula, Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Wabunge, viongozi wa Dini na viongozi wa taasisi mbalimbali.

Akizungumza baada ya kiapo hicho, Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Dkt. Mpango kwa kushika wadhifa huo wa Makamu wa Rais na ameeleza kuwa baada ya kupitia majina mbalimbali ameona Dkt. Mpango anafaa kushika wadhifa huo kutokana na uchapakazi wake, umahiri, ucha Mungu na utulivu.

Amebainisha kuwa kutokana na sifa hizo anatarajia pamoja na majukumu mengine Dkt. Mpango atamsaidia katika uchumi, udhibiti wa fedha za Serikali na kwa kuwa masuala ya Muungano yapo katika Ofisi yake atashughulikia ajenda iliyokwama ya uhusiano wa kifedha katika Muungano.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Mpango amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa imani yake kwake na ameahidi kuwa atakuwa msaidizi mwaminifu na mtiifu kwa Mhe. Rais na nchi ya Tanzania.

Ameongeza kuwa yupo tayari kuchapakazi mchana na usiku, kushirikiana na viongozi wengine na amesisitiza kuwa Watanzania hawana hofu na uongozi wa Mhe. Rais Samia.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wamempongeza Mhe. Dkt. Mpango kwa kushika wadhifa huo na wameahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *