TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja na kuwa Utamaduni hutangaza mila na desturi za nchi lakini pia ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato kwasababu ni moja ya vivutio vya utalii.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 08 Septemba, 2021 Jijini Mwanza wakati akifunga Tamasha la Utamaduni lililoandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania.

Kufuatia umuhimu wa Utamaduni, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imejipanga kupanua wigo wa vivutio vya utalii , ukiwemo utalii wa utamaduni ambapo tayari ameanza kuchukua hatua za kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii, biashara na uwekezaji nchini kupitia filamu inayoendelea kurekodiwa na Kipindi maarufu cha Royal Tour

Mhe. Rais Samia amewaomba Machifu hao nchini kwa kushirikiana na Serikali kudumisha amani na usalama ikiwa ni pamoja na kusuluhisha migogoro kwenye jamii zinazowazunguuka.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewasihi viongozi hao wa kimila kuwahimiza Watanzania kujilinda na janga la UVIKO 19 ikiwa ni pamoja na kupata chanjo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewaomba viongozi hao wa kimila  kuwahamaisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa litakalofanyika mwakani 2022.

Katika Tamasha hilo, Machifu wamemtawaza Mhe. Rais Samia kuwa Chifu Mkuu wa Machifu wote nchini na kumpa jina la Chifu Hangaya likiwa na maana ya Nyota ya asubuhi inayong’aa.

Mara baada ya kutawazwa kuwa Chifu Mkuu Hangaya, Mhe. Rais Samia amewashukuru Machifu hao kwa heshima waliyompa na kuwaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mhe. Rais Samia mara baada ya kuhudhuria Tamasha hilo la Utamaduni amerejea Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *