TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema ulemevu hauzuii kufanya mambo makubwa duniani kwasababu binadamu tunatofautiana umbo lakini maumbile sote tupo sawa hivyo hali hiyo sio kikwazo cha msingi bali inapaswa kutayarisha mazingira, kutoa uwezo wa kuelimisha ili kila mtu aweze kufanya kila kitu.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 07 Desemba, 2021 katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam kuipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors) baada ya kufuzu kwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yatakayo fanyika nchini Uturuki mwaka 2022.

Aidha, Mhe. Rais ametolea mfano washiriki wa mashindano ya urembo kwa viziwi na watanashati barani Afrika ambao walifanya vizuri na kusema Serikali haitaacha mtu yeyote nyuma katika maendeleo bila kujali hali yake ya maumbile au ulemavu wa viungo.

Mhe. Rais Samia pia amekipongeza Chama cha Mpira wa Miguu wa Watu Wenye Ulemavu (TAFF), Kamati ya Maandalizi na Wachezaji wa timu hiyo pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mafanikio mbalimbali yaliyopatikana.

Mhe. Rais amewataka wachezaji wa Tembo Warriors kutobweteka na hatua waliyofikia bali waongeze bidiii ili wapate ushindi zaidi katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia nchini Uturuki.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema mafanikio ya timu ya Tembo Warriors ni ushuhuda wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ambayo inaitaka sekta ya michezo kuwa miongoni mwa sekta itakayotoa ajira kwa vijana.

Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kuangalia namna bora ya wachezaji wa timu hiyo kukaa pamoja kwa ajili ya maandalizi ya muda mrefu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika michuano hiyo ya kombe la dunia.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amemkabidhi Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim Tuzo ya Heshima ya Utatuzi wa Migogoro, Demokrasia na haki za Binadamu aliyotunukiwa na Taasisi ya Kemet Butros Ghali (KBG) ya nchini Misri.

Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa Taasisi hiyo iliamua kumpatia Dkt. Salim Tuzo hiyo ili kuenzi mchango wake katika Uongozi wa Umoja wa Afrika (OAU) kuanzia mwaka 1989 – 2001. Pia kwa kuonyesha jitihada kubwa za kusaidia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kupigania haki, usawa, umoja, kudumisha ulinzi na usalama katika kuleta maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Taasisi ya KBG imekuwa na utaratibu wa kutoa tuzo mbalimbali kila mwaka na kutambua michango ya watu katika tafiti, elimu, amani, demokrasia pamoja na kujishughulisha na masuala ya kuleta amani na ujuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *